Habari Za Kimataifa

Waaga dunia baada ya kusombwa na mafuriko
Waaga dunia baada ya kusombwa na mafuriko

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Misaada ya Kibinadamu (OCHA) imesema watu wasiopungua 17 wameaga dunia baada ya kusombwa na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha nchini Somalia. Taarifa iliyotolewa jana Jumatano na OCHA imesema watu zaidi ya 370,000 wamelazimika kuyahama makazi yao kutokana na athari za mvua na mafuriko hayo katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika hususan katika wilaya ya Belet Weyne.

Taasisi hiyo ya UN imebainisha kuwa, maeneo yaliyoathiriwa zaidi na mafuriko hayo ni majimbo ya Hirshabelle, Jubaland na Kusini Magharibi, ambapo mashamba ya kilimo, miundombinu na mabarabara yameharibiwa na majanga hayo ya kimaumbile.

Haya yanajiri siku chache baada ya watu wengine 15 kupoteza maisha katika ajali ya kuzama boti katika mji wa Beledweyn katikati ya Somalia.

Wakati huohuo, Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) limesema kuwa linahitaji msaada wa dola milioni 10 za Marekani ili kukidhi mahitaji ya dharura ya watoto walioathiriwa na mafuriko nchini Sudan Kusini. Mjumbe wa UNICEF nchini humo Mohamed Ayoya amesema, zaidi ya watu laki 9 wakiwemo watoto 490,000 wanahitaji msaada wa haraka wa kibinadamu.

Nchini Tanzania idadi ya watu waliofariki dunia kutokana na mvua inakadiriwa kuwa 40 na katika nchi jirani ya Kenya watu takribani 30 nao pia wamepoteza maisha kufuatia mafuriko. Watabiri wa hali ya hewa wanatarajia mvua hizo kubwa zitaendelea kunyesha hadi mwezi Disemba.

November 8,2019

Bosco Ntaganda ahukumiwa miaka 30 gerezani
Bosco Ntaganda ahukumiwa miaka 30 gerezani

Mahakama ya kimataifa ya uhalifu imemhukumu kifúngo cha miaka 30 gerezani, mbabe wa zamani wa kivita katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo Bosco Ntaganda, kwa makosa ya ukatili, ikiwa ni pamoja na mauaji, ubakaji na kuwatumikisha watoto jeshini.

Ntaganda mwenye umri wa miaka 46, alikutwa na hatia Julai 18 kuhusiana na vitendo vya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu, vilivyofanyika wakati alipokuwa kiongozi wa kijeshi wa kundi la wapiganaji la Union des Patriots Congolais (UPC),-Umoja wa Wazalendo wa Congo, mashariki mwa Congo kati ya 2002 hadi 2003.

Wakati akisoma hukmu hiyo, jaji wa mahkama ya ICC Robert Fremr, amesema uhalifu aliohukumiwa Ntaganda, licha ya ukubwa wake na kiwango chake cha kulaumika, hakustahili kifungo cha maisha gerezani. Mkuu wa Ntaganda, kiongozi wa chama cha UPC Thomas Lubanga, anatumikia kifungo cha miaka 14 gerezani baada ya kutiwa hatiani na ICC kwa kuandikisha na kutumikisha watoto jeshini

November 8,2019

Maelfu wakosa makazi sababu ya mafuliko
Maelfu wakosa makazi sababu ya mafuliko

Mafuriko yaliyoyaathiri maeneo ya kusini mashariki mwa Niger tangu mwanzoni mwa mwezi Oktoba hadi sasa yamesaabisha watu elfu 23 kukosa makazi.

Ukame wa mwaka jana ulioikumba Niger na mafuriko yaliyoyaathiri maeneo ya kusini mashariki mwa nchi hiyo umezidisha mgogoro wa kibinadamu katika nchi hiyo ambayo mara kwa mara imekuwa ikilengwa na mashambulizi ya magaidi wa Boko Haram.

Ripoti ya mwezi Septemba mwaka huu ya vyombo vya habari vya serikali ya Niger inaeleza kuwa, kuongezeka kiwango cha maji ambacho hakijawahi kushuhudiwa nchini humo katika kipindi cha miaka 50 iliyopita kumesababisha maafa makubwa katika mji mkuu Niamey. Watu 57 wameaga dunia katika mafuriko hayo. Nigeri inapatikana magharibi mwa Afrika huku asilimia 80 ardhi ya nchi hiyo ikiwa ni jangwa. Niger ilipata rasmi uhuru wake mwaka 1960 kutoka kwa mkoloni Ufaransa.

October 22/2019

Waziri Mkuu Boris Johnson apata pigo jingine
Waziri Mkuu Boris Johnson apata pigo jingine

Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson amepata pigo jingine, jioni ya leo baada ya spika wa bunge la Uingereza John Bercow kuamuru kuwa serikali yake haiwezi kuwataka wabunge kupigia kura tena makubaliano ya Brexit.

Boris Johnson alifanya jaribio la pili kuwataka wabunge waunge mkono makubaliano yake na Umoja wa Ulaya juu ya mchakato wa Uingereza kujiondoa katika umoja huo - Brexit.

Zikiwa zimesalia siku 10 pekee kabla ya tarehe ambayo Uingereza inapaswa kuondoka Umoja wa Ulaya- Oktoba 31, serikali ya Johnson ilinuia kulishinikiza bunge kuupigia kura mpango wake kwa kuukubali kama ulivyo au kuukataa bila ya kuufanyia marekebisho. Juhudi za Johnson zinajiri siku mbili baada ya wabunge kupiga kura kutaka muda zaidi ya tarehe ya sasa ya kufanya maamuzi ya mchakato wa Brexit.

October 22/2019

Wahamiaji wadaiwa kuwa na magonjwa ya kuambukiza
Wahamiaji wadaiwa kuwa na magonjwa ya kuambukiza

Serikali ya Libya imewahamishia nchini Misri makumi ya wahamiaji haramu wanaodaiwa kuwa na magonjwa ya kuambukiza.

Idara ya Kusimamia Uhamiaji katika mji wa mashariki wa Benghazi nchini Libya imeripoti kuwa, wahamiaji haramu 95 wamepelekwa nchini Misri kwa kutumia usafiri wa mabasi.

Siku ya Jumatatu, idara hiyo iliwahamishia katika nchi za Nigeria na Misri wahamiaji haramu wengine zaidi ya 100.

Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) limeripoti kuwa, kuna wakimbizi na wahamiaji haramu 650,000 nchini Libya, ambapo 6,000 miongoni mwao wakiwemo wanawake na watoto wadogo wanazuiliwa katika vituo mbalimbali.

October 18, 2019

Rwanda iko tayari kuwapa hifadhi wakimbizi 30,000
Rwanda iko tayari kuwapa hifadhi wakimbizi 30,000

Kwa mujibu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR), Rwanda imewapokea wakimbizi 189 kutoka Libya kufikia sasa.

Serikali ya Rwanda imesema iko tayari kuwapokea na kuwapa hifadhi wakimbizi 30,000 kutoka Libya lakini itawakaribisha kwa utaratibu maalumu na katika hatua kadhaa, ili kuzuia nchi hiyo yenye watu milioni 12 isiwe na mzigo.

October 18, 2019

Polisi wamewakamata takribani waandamanaji 100
Polisi wamewakamata takribani waandamanaji 100

Polisi wamesema wamewakamata takribani waandamanaji 100 tangu kuibuka kwa maandamano jimboni Catalonia siku ya jumatatu.

Maandamano hayo yalisababishwa na kufungwa jela kwa kiongozi wa wanaotaka kujitenga katika jimbo hilo.

Akizungumza katika mkutano na wanahabari, Kaimu waziri wa mambo ya ndani wa Uhispania Fernando Grande-Marlaska amesema, hakutakuwa na msamaha kwa watu hao.

Marlaska ameongeza kuwa serikali itachukua hatua zote zinazostahili ili kuhakikisha usalama wa Catalonia. Awali waziri huyo wa mambo ya ndani wa Uhispania alisema, Madrid itatuma polisi zaidi Catalonia ili kuhakikisha usalama na kuwaruhusu polisi wa jimbo hilo kupata mapumziko.

October 18, 2019

Kwa mara nyengine watu 109 waokolewa baharini
Kwa mara nyengine watu 109 waokolewa baharini

Meli ya uokoaji ya "Ocean Viking" imewaokoa kwa mara nyengine watu 109 waliokuwa wanahitaji msaada wa dharura katikati ya bahari. Shirika la misaada la SOS katika bahari ya Mediterenia pamoja na lile la Madaktari wasiokuwa na mipaka yamesema kuwa hatua ya awali ilikuwa kuwachukua watu 48 waliokuwa kwenye boti ya mbao karibu kilomita mia moja kaskazini mwa pwani ya Libya.

Baadae iliwaokoa watu wengine sitini na mmoja waliokuwa kwenye mtumbwi. Kwa sasa haijabainika meli hiyo ya "Ocean Viking" itatua katika bandari gani. Mwishoni mwa wiki meli hiyo ilikubaliwa kuwapeleka Lampedusa watu 82 iliyokuwa imewaokoa katikati ya bahari.

September 18/2019

Hatimaye Tunisia yafanya uchaguzi huru
Hatimaye Tunisia yafanya uchaguzi huru

Wananchi wa Tunisia juzi Jumapili, Septemba 15, 2019 walishiriki kwenye uchaguzi muhimu sana wa Rais ambao ulikuwa wa pili huru baada ya wananchi hao kumpindua dikteta wa muda mrefu wa nchi hiyo, Zine el Abidine Ben Ali mwaka 2011.

Uchaguzi huo uliowashirikisha wagombea 24 umefanyika kwa usalama na amani. Matokeo ya awali yameonesha kwamba, wagombea wawili Kaïs Saïed, wa kujitegemea, na Nabil Karoui wa chama cha 'Qalb Tounes' ndio walioingia duru ya pili ya uchaguzi huo kwa kupata asilimia kubwa zaidi ya kura ikilinganishwa na wagombea wengine.

Uchaguzi wa rais nchini Tunisia ulikuwa ufanyike tarehe 17 Novemba mwaka huu wa 2019, lakini imebidi ufanyike kabla ya wakati wake kufuatia kifo cha Beji Caid Essebsi rais wa zamani aliyetawala Tunisia tangu mwaka 2014. Essebsi alifariki dunia tarehe 25 Julai mwaka huu wa 2019 akiwa na umri wa miaka 92.

Baadhi ya wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, kujitokeza idadi kubwa ya wagombea kwenye uchaguzi huo wa juzi Jumapili ni ishara ya kuanza kuota mizizi na kuimarika misingi ya demokrasia nchini Tunisia. Wataalamu mbalimbali wakiwemo wahadhiri wa Sayansi Jamii wanaona kuwa ni jambo lililo mbali kutokea machafuko na kukanyagwa misingi ya demokrasia nchini Tunisia.

September 18/2019

Uhispania yajiandaa kurudi katika uchaguzi
Uhispania yajiandaa kurudi katika uchaguzi

Uhispania inajianda kurudi katika uchaguzi uliopangwa kufanyika Novemba 10 mwaka huu ikiwa ni mara ya nne ndani ya kipindi cha miaka minne.Hatua hiyo inakuja baada ya kiongozi wa serikali kutoka chama cha Kisoshalisti, Pedro Sanchez. kushindwa kupata uungwaji mkono wa kutosha kwa kuendelea kushikilia nafasi yake.

"Nchi imekaribia (kuandaa) uchaguzi mpya mnamo Novemba 10," Sanchez amekiri Jumanne wiki hii baada ya kupokelewa na Mfalme wa Uhispania Felipe wa 6, ambaye alikuwa akifanya mazungumzo tangu Jumatatu, ili kutafutia ufumbuzi swala hilo."Matokeo (ya mazungumzo ya mfalme) yako wazi: hakuna wingi wa viti katika bunge la taifa ambao unaweza kupelekea kuundwa kwa serikali," ameongezea Bw Sanchez, ambaye alishinda uchaguzi uliopita wa Aprili 28 lakini bila kupata wingi wa viti bungeni.

"Nilijaribu kwa njia zote lakini kazi yangu iliambulia patupu," Bw Sanchez ameongeza, akimaanisha wapinzani wake ambao walimshtumu tangu mwanzo kwamba anataka uchaguzi mpya.Uhispania inaendelea kukumbwa na ukosefu wa utulivu wa kisiasa tangu kuvujinka kwa muungano wa vyama viwili vyenye wafuasi wengi mnamo mwaka wa 2015 na kuingia katika Bunge chama cha mrengo wa kushoto chenye itikadi kali cha Podemos na kile cha Ciudadanos. Kwa sasa Bunge la Uhispania Bunge limegawanyika.

September 18/2019

Mwili wa Robert Mugabe umewasili nchini Zimbabwe
Mwili wa Robert Mugabe umewasili nchini Zimbabwe

Mwili wa aliyekuwa Rais wa Zimbabwe,Robert Mugabe umewasili nchini Zimbabwe kutokea Singapore, ambapo alifariki juma lililopita akiwa na miaka 95.Mugabe, alikuwa kiongozi wa kwanza wa nchi hiyo tangu ilipopata uhuru mwaka 1980. Alikuwa madarakani kwa karibu miongo minne kabla ya kuondolewa madarakani kwa mapinduzi mwaka 2017.Atazikwa siku ya Jumapili baada ya shughuli za maziko siku ya Jumamosi.

Mwili wa Mugabe umepelekwa kwenye makazi ya familia ''Blue Roof'' mjini Harare Siku ya Alhamisi na Ijumaa, Mwili wa Mugabe utalala katika uwanja wa mpira wa Rufaro eneo la Mbare mjini Harare, ambapo ndipo alipoapishwa kuwa waziri mkuu wa kwanza wa Zimbabwe baada ya kupatiwa uhuru kutoka kwa koloni la kiingereza mwaka 1980.

Taratibu za kitaifa za kuuaga mwili wake zitafanyika siku ya Jumamosi ,kwenye uwanja wenye uwezo wa kupokea watu 60,000 kabla ya kuzikwa kijijini kwao Jumapili.

Rais wa taifa hilo Emmerson Mnangagwa ametaja kuwa ''shujaa wa taifa'' kwa jitihada zake za kuisaidia Zimbabwe kupata uhuru wake.Lakini ripoti zinasema kuwa Mugabe hakutaka waliomuondoa madarakani kushiriki katika maziko yake, hivyo badala yake huenda shughuli za maziko zikafanywa kwenye makazi ya familia yake.

September 12/2019

Waziri Mkuu Uingereza atakiwa kufungua bunge
Waziri Mkuu Uingereza atakiwa kufungua bunge

Wabunge wa vyama vya upinzani nchini Uingereza wamemtaka Waziri Mkuu Boris Johnson alifungue bunge, baada ya mahakama ya juu nchini Scotland kuamua kwamba hatua aliyoichukua wiki iliyopita ya kusimamisha shughuli za bunge ilikwenda ikinyume cha sheria. Mahakama hiyo ilitoa hukumu lakini haikuamuru kubatilishwa kwa hatua ya kusimamishwa bunge.

Mahakama hiyo ya Scotland pia imesema uamuzi wa mwisho unapaswa kupitishwa na mahakama ya juu ya Uingereza. Suala hilo litaanza kusikilizwa Jumanne wiki ijayo. Mbunge wa chama cha Scottish National Party, SNP Joanna Cherry amesema amefurahishwa sana na hukumu hiyo.

Amesema uamuzi huo ni ujumbe kwa Waziri Mkuu Johnson kwamba hawezi kuvunja sheria bila ya kuwajibishwa.Waziri kivuli wa masuala ya Brexit Keir Starmer amesema hatua ya kulisimamisha bunge ilikuwa ya makosa.

Katika mahojiano na shirika la utangazaji la BBC jana Jumanne, Johnson alisisitiza kwamba mapumziko hayo ya bungeniya kujiandaa kwa ajili ya kutoa vipaumbele katika sekta za elimu, huduma za afya na usalama katika vikao vijavyo vya bunge.

September 12/2019

40 wanahofiwa kuaga dunia kwa kuzama majini Libya
40 wanahofiwa kuaga dunia kwa kuzama majini Libya

Takribani watu 40 wanahofiwa kuaga dunia kwa kuzama majini katika ufukwe wa Libya kufuatia kuzama kwa boti ya wahamiaji kuzama katika bahari ya Mediterania.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi limesema tukio hilo la Jumanne limeifanya irejelee wito wake wa haraka wa kuchukua hatua za kuokoa maisha.

Manusura wapatao 60 wameokolewa na kupelekwa ufukweni katika mji wa pwani wa Al-Khoms, takribani kilomita 100 mashariki mwa Tripoli. Shughuli ya uokoaji iliyofanywa na walinzi wa pwani ya Libya pamoja na wavuvi imekuwa ikiendelea tangu asubuhi ya leo na bado inaendelea.

Vincent Cochetel, mwakilishi maalumu wa UNHCR katika eneo la Mediterania ya kati amesikitishwa na maafa hayo na ametaka hatua zichukuliwe kuyazuia katika siku za usoni.

Timu za UNHCR zimenawapatia manusura msaada wa matibabu na wa kibinadamu. Tukio hili limekuja wiki chache baada ya tukio lingine la kuzama kwa meli ambapo maisha ya watu 150 yanakadiriwa kupotea katika tukio moja tu kwa mwaka huu katika bahari ya Mediterania.

Kufuatia janga la jana, inakadiriwa kuwa watu 900 tayari wamepoteza maisha wakijaribu kuvuka bahari ya Mediterania kwa mwaka huu wa 2019.

August 28/2019

Watu wasiopungua 37 wauawa Sudan
Watu wasiopungua 37 wauawa Sudan

Vyombo vya habari vya Sudan vimeripoti kuwa watu wasiopungua 37 wameuawa katika mapigano ya kikabila yaliyotokea mashariki mwa nchi hiyo.

Gazeti la Sudan Tribune limeripoti leo kuwa, mbali na watu 37 waliouawa, 200 wengine wamejeruhiwa katika mapigano kati ya makabila ya Bani Amer na Nuba mashariki mwa nchi hiyo. Hata hivyo chanzo hasa cha mapigano hayo bado hakijajulikana.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, majeruhi wa mapigano hayo wamekimbizwa hospitalini.

Katika radiamali na hatua liliyochukua kuhusiana na mapigano hayo ya kikabila, siku ya Jumapili, Baraza la Utawala la Sudan lilitangaza hali ya hatari katika jimbo la Bahari Nyekundu na kumwachisha kazi Gavana na Naibu Mkuu wa vyombo vya usalama katika jimbo hilo kwa kuzembea kuchukua hatua za kuzuia kutokea mapigano hayo.

Baraza hilo aidha limeamuru ufanyike uchunguzi kuhusu mapigano hayo na kusisitiza kuwa litawachukulia hatua waliosababisha kutokea kwake.

Mapigano hayo ya kikabila kati ya kabila la Bani Amer na lile la Nuba yalianza siku ya Alkhamisi iliyopita katika bandari ya Sudan makao makuu ya jimbo la Bahari Nyekundu...

August 28/2019

Sudani kurudi katika utawala wa kiraia
Sudani kurudi katika utawala wa kiraia

Viongozi wa kijeshi nchini Sudani na muungano wa makundi ya upinzani wameunda rasmi baraza huru litakaloiongoza nchi hiyo kurudi kwenye utawala wa kiraia.Baraza hilo litaiongoza Sudani katika kipindi cha mpito cha miaka mitatu.Luteni Jenerali Abdel Fattah Abdelrahman Burhan ataliongoza baraza hilo kwa siku za awali. Wajumbe wa baraza ni raia sita na maafisa wa ngazi za juu watano wa jeshi.

Jenerali Burhan ndiye aliyechukua hatamu za uongozi baada ya jeshi kumng'oa Raisi Omar al-Bashir madarakani.Baraza hilo linatarajiwa kuapishwa Jumatano (leo) asubuhi.

Waziri Mkuu pia anatarajiwa kuapishwa hii leo pia.Hatua hiyo ilitangazwa na msemaji wa wa Baraza la Mpito la Kijeshi (TMC).

TMC ndiyo ilichukua mamlaka kutoka kwa Bashir mwezi April. Tokea hapo Sudan imeshuhudia maandamano ya kidemokrasia na pia mashambulizi makali ya waandamanaji kutoka kwa vyombo vya usalama.

Wanamgambo wanaoongozwa na Hemeti (RSF) - ambao wametokana na kundi la Janjaweed ambalo linatuhumiwa kutekeleza mauaji katika jimbo la Darfur - wamekuwa wakilaumiwa kwa ghasia za hivi karibuni.Ghasia hizo ni pamoja na mauaji ya Juni 3 ambapo watu 120 wanaripotiwa kuuawa, na wengi wao kutupwa kwenye mto Nile.Hata hivyo viongozi wa RSF wamekanusha kupanga

August 21,2019

Apigwa risasi baada ya kuwateka watu 16
Apigwa risasi baada ya kuwateka watu 16

Mtu aliyekuwa na silaha na kuwashikilia mateka karibu abiria 16 mjini Rio de Janeiro leo, amepigwa risasi na kufariki, wakati polisi walipokuwa wakijadiliana nae wakijaribu kumaliza mkwamo huo.

Kiasi watu sita, wanawake wanne na wanaume wawili, wameachiwa huru hadi sasa kutoka katika basi hilo ambalo lilisimama katika daraja ambalo hutumika sana linalounganisha mji wa Rio na mji wa jirani wa Niteroi.

Polisi waliokuwa na silaha kali ikiwa ni pamoja na jeshi na walenga shabaha walilizunguka basi hilo wakati wakijadiliana na mtu huyo mwenye silaha , ambae kituo cha habari cha G1 News kimeripoti kuwa alikuwa na silaha, na chombo chenye petroli. Mtu huyo anasemekana alipanda basi hilo linaloelekea Rio asubuhi leo na kuanza kuwatishia abiria.

August 21,2019

Watatu wameuawa kwa kupigwa risasi na polisi
Watatu wameuawa kwa kupigwa risasi na polisi

Watu watatu wameuawa jana Jumatatu, Agosti 19 kwa kupigwa risasi na polisi wakati wa maandamano ya kupinga ukosefu wa usalama katika eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ambapo visa vya mauaji vimekithiri, kwa mujibu wa vyanzo rasmi.

Mkuu wa wilaya ya Beni katika mkoa wa Kivu Kaskazini, ameliambia shirika la habari la AFP kuwa mvulana mdogo wa takriban miaka 25 ambaye amepigwa risasi tumboni, amefariki baada ya kufikishwa hospitalini; na mtu mwengine kutoka jamii ya Mamburikimo amepigwa risasi, na kufariki papo hapo.

Hali ya usalama katika eneo hilo la Mashariki mwa DRC, si shwari. Usalama umekuwa ukidorara kila mara, huku visa vya mauaji vikiendelea kuongezeka.

Kundi la waasi wa Uganda la ADF limekuwa likinyooshewa kidole cha lawama kwamba linahusika na mauaji hayo.Lakini wadadisi wanasema kwamba kundi hlo limekuwa likishirikiana na makundi mengine ya raia wa DRC wanaobebelea silaha kwa kuzorotesha usalama katika eneo hilo.

August 20/2019

Misri imewahukumu kifo washitakiwa sita
Misri imewahukumu kifo washitakiwa sita

Mahakama nchini Misri imewahukumu kifo washitakiwa sita na wengine 41 kutumikia kifungo cha maisha grezani baada ya kuwatia hatiani kwa makosa ya ugaidi. Katika hukumu hiyo ya leo, mahakama hiyo pia imeamuru kifungo cha miaka 15 gerezani wa washitakiwa wengine saba, huku mtoto mmoja akifungwa miaka mitatu na pia ikawafutia mashtaka washukiwa wengine 14 katika kesi hiyo. Kesi hiyo iliwahusisha washtakiwa 70 ambapo mmoja kati yao alifariki dunia.

Hukumu zote zinaweza kukatiwa rufaa. Watu hao walishtakiwa kwa kuunda kundi katika wilaya mbili za Krdasa na Nahia karibu na Cairo kwa lengo la kuzuia taasisi za serikali kutekeleza shughuli zake kwa matumizi ya ugaidi na ghasia. Pia wameshtakiwa kwa mauaji ya watu watatu ikiwa ni pamoja na afisa wa polisi na kumiliki silaha.

August 20/2019

Akiri kwamba alipokea rushwa
Akiri kwamba alipokea rushwa

Rais aliyeondolewa madarakani wa Sudan amekiri kwamba alipokea rushwa kutoka kwa Mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia Muhammad bin Salman.

Katika kikao cha kwanza cha kesi yake iliyofanyika leo mjini Khartoum, Rais aliyeondolewa madarakani wa Sudan, Omar al Bashir amefichua kwamba, mamilioni ya dola za Marekani yaliyokutwa nyumbani kwake baada ya kupinduliwa alipewa na mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia, Muhammad bin Salman na Rais wa Imarati, Khalifa bin Zayed.

Al Bashir ambaye anakabiliwa na tuhuma za ufisadi na kuua waandamanaji amekiri kwamba, alipokea fedha taslimu dola milioni 90 kutoka kwa mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia Muhammad bin Salman.Amesema fedha hizo zilikabidhiwa kwake kupitia wajumbe kadhaa wa Saudia kutoka kwa Bin Salman. Vilevile amesema alipokea dola nyingine milioni moja kutoka kwa Rais wa Imarati, Khalifa bin Zayed.

Al Bashir alikuwa mshirika mkubwa wa Saudi Arabia na Imarati katika vita vya kidhalimu dhidi ya watu wa Yemen na mamia ya askari wa Sudan waliotumwa na Omar al Bashir huko Yemen kuizisaidia nchi hizo mbili, wamueawa wakipigana vita.

August 20/2019

Mwanamke mmoja aua watu sita
Mwanamke mmoja aua watu sita

Mwanamke mmoja ameua watu sita magharibi mwa Chad baada ya kujilipua kwa bomu ambalo alikuwa amejifunga. Shambulio hilo linadaiwa kufanywa na wanamgambo wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram.

Afisa wa jeshi wa ngazi ya juu ameeleza kuwa watu 6 wamepoteza maisha akiwemo mwanajeshi mmoja katika shambulio hilo la kujilipua kwa bomu lililofanywa na mwanamke huyo katika wilaya ya Kaiga-Kindjiria.

Watu wengine kadhaa wamejeruhiwa pia katika shambulio hilo la kigaidi. Wilaya ya Kaiga-Kindjiria inapatikana katika mkoa wa Lac karibu na Ziwa Chad.

Tangu mwaka 2018 hadi sasa kundi la Boko Haram limefanya mashambulizi yasiyopungua kumi karibu na mpaka wa Chad; ambayo mengi yalikusudiwa kuzilenga kambi za jeshi.

Mwezi Machi mwaka huu, wanajeshi 23 wa Chad waliuawa baada ya kambi yao huko Ziwa Chad kushambuliwa na wanamgambo wa Boko Haram. Aidha watu wasiopungua 27,000 wameuawa Nigeria katika mashambulizi ya kundi hilo la kigaidi na wengine milioni mbili wamelazimika kuwa wakimbizi.

August 16,2019

Watu 14 wameuawa mapigano kati ya jeshi na waasi
Watu 14 wameuawa  mapigano kati ya jeshi na waasi

Karibu watu 14 wameuawa leo Alhamisi mashariki mwa Burma katika mapigano kati ya jeshi na makundi ya waasi.

Mapigano hayo yametokea kwa mara ya kwanza katika shule ya kijeshi.

Mashambuliz matano yalitekelezwa na makundi ya waasi wa kikabila Alhamisi asubuhi katika mji wa Pyin Oo Lwin, mji wa kitalii karibu na Mandalay ambapo kunapatikana kambi kadhaa za jeshi. Shule ya kijeshi imelengwa hasa na roketi.

Jeshi limejibu mashambulizi hayo kwa kuzindua operesheni dhidi ya makundi hayo.

Mwandishi wa habari wa shirika la habari la AFP ameshuhudia miili ya askari saba na polisi wanne katika kituo cha polisi kilichoshambuliwa.

Jeshi la Kitaifa la Ukombozi la Taaung (TNLA), moja ya makundi makubwa ya waasi kaskazini mashariki mwa nchi hiyo, limedai kuhusika na mashambulizi hayo kwa kulipiza kisasi kwa operesheni za jeshi."

August 16,2019

Ndege aina ya Airbus A321 ya urusi yatua kwa dharula
Mwanamke mmoja aua watu sita

Urusi imekaribisha hatua ya kishujaa na ya kushangaza ya marubani wa ndege aina ya Airbus A321, ambao walilazimika kutua kwa dharura Alhamisi katika shamba la mahindi. Ndege hiyo ambayo iligonga kundi la ndege angani, ilikuwa imeabiri watu 233.Mapema asubuhi ya jana , ndege ya shirika la ndege la Urusi la Ural Airlines iliondoka kutoka uwanja wa ndege wa Zhukovsky, katika kitongoji cha mji mkuu Moscow, kuelekea Simferopol, mji mkuu wa rasi ya Ukraine ya Crimea uliounganishwa na Urisi mnamo mwaka 2014.

Lakini wakati wa kuondoka, ndege hiyo iliokuwa imeabiri watu 226 na wafanyakazi 7 "iligonga kundi la ndege", ambapo ndege kadhaa zilijikuta katika injini za chombo hicho cha Airbus na kusababisha "usumbufu mkubwa katika safari yake, "kwa mujibu wa mamlaka ya safari za anaga nchini Urusi, Rosaviatsia.

Wafanyikazi wa ndege hiyo waliamua kutua kwa dharura "katika chamba wa mahindi (...) linalopatikana zaidi ya kilomita moja kutoka eneo la ndege kupaa angani," mamlaka ya safari za anga nchini Urusi imebaini, huku ikibaini kwamba hakuna hasara kubwa iliyotokea upande wa abiria, ispokuwa abiria 23 pekee ambao wamejeruhiwa.

Watu 23 wakiwemo watoto 9 wamejeruhiwa katika tukio hilo la kushangaza, kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Urusi. Ishirini na mbili kati yao walipewa huduma ya matibabu kabla ya kuruhusiwa kwenda nyumbani, wakati mwanamke mmoja mwenye umri wa miaka 69 alilazwa hospitalini, wizara hiyo imesema katika taarifa.

August 16,2019